Thursday, 11 August 2016

Kitwanga Akutana Uso Kwa Uso na Rais Magufuli

Rais John Magufuli jana alikutana ana kwa ana na rafiki yake, Charles Kitwanga ikiwa ni siku 80 baada ya kumvua cheo cha Waziri wa Mambo ya Ndani kwa kosa la kuingia bungeni kujibu maswali akiwa amelewa. 

Wawili hao walikutana kwenye Jimbo la Misungwi ambako Rais alisimama akitokea Wilaya ya Sengerema ambako alihutubia wananchi. 

Rais alitengua uteuzi wa Kitwanga Mei 20, wakati sakata la utekelezwaji mbovu wa mkataba wa Sh37 bilioni baina ya Jeshi la Polisi na kampuni ya Lugumi Enterprises likivuma kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano. 

Lakini jana, hali ilionekana ya kikazi zaidi wakati Rais alipofika kwenye jimbo hilo. Kitwanga, ambaye ni mbunge wa Misungwi mkoani Mwanza, alitumia nafasi hiyo kukutana na Rais kwa mara ya kwanza hadharani, kuwasilisha kero za wananchi wake, hasa ya maji. 

Katika tukio hilo lililovutia hisia za waliokuwepo, Rais aliuthibitishia umma kuwa yeye na Kitwanga ni marafiki wa muda mrefu, alipokuwa akijibu ombi la mbunge huyo la kutaka Serikali itatue kero ya maji eneo la Usagara na Misungwi. 

“Kitwanga ni rafiki yangu. Tayari Serikali imepanga kutumia zaidi ya Sh8 bilioni kutekeleza mradi mkubwa wa maji maeneo ya jimbo la Misungwi, ikiwemo Usagara,” alisema Rais Magufuli akiwa amesimama kwenye gari lililofunuliwa upande wa juu. 

Katika sakata la Lugumi, wabunge walitaka suala lijadiliwe baada ya taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kubaini kuwa kampuni hiyo ilishindwa kufunga mashine za kielektroniki za kuchukulia alama vidole kwa mujibu wa mkataba. 

Mkataba huo ulisainiwa mwaka 2011 lakini hadi CAG alipokuwa akifanya ukaguzi mwaka jana, ni vituo 14 tu kati ya 118 vilivyokuwa vimefungwa mashine hizo, huku Lugumi Enterprises ikiwa imelipwa Sh36 bilioni ambazo ni zaidi ya asilimia 90 ya fedha za mkataba huo. 

Kitwanga alihusishwa na sakata hilo kutokana na dhamana yake na pia kuwa na hisa kwenye kampuni ya Infosys, ambayo ni wakala wa kampuni ya Dell inayozalisha kompyuta, kuhusishwa kutoa vifaa hivyo. 

Hata hivyo, Juni 22, Kitwanga aliwaambia waandishi wa habari nyumbani kwake kuwa Infosys haina uhusiano wowote wa kibiashara na Lugumi.

Jitihada za wabunge, hasa wa upinzani kutaka kuzungumzia suala hilo zilikwama kwa maelezo ya kutaka kusubiri ripoti ya kamati ndogo iliyoundwa kuchunguza suala hilo. 

Ripoti hiyo iliwasilishwa mwishoni mwa vikao vya Bunge la Bajeti na haikujadiliwa baada ya Naibu Spika, Dk Tulia Ackson kusoma maagizo ya Bunge kwa pande zinazohusika kwenye mkataba. 

Kabla ya suala hilo kuzuiwa kujadiliwa, wabunge walikuwa wakidai kuwa Rais na Kitwanga ni marafiki wa karibu na baadaye mitandao ya kijamii ikasambaza mkanda unaoonyesha jinsi walivyokuwa wakijadili suala la Magufuli kuchukua fomu ya kugombea urais. 

Kwenye kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, Magufuli alimnadi Kitwanga kwa kueleza kuwa anamfahamu kwa kuwa walisoma wote na ni rafiki yake. 

Kabla ya kwenda Sengerema kwa kivuko jana, Rais alihutubia wilayani Sengerema ambako aliendelea na onyo lake dhidi ya watu anaosema wanataka kuvuruga amani.

Akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Mnadani mjini Sengerema, Rais Magufuli aliwataka wenye lengo la kuvuruga amani kumsubiri amalize kipindi chake cha uongozi kwa sababu hatawapa fursa hiyo. 

“Wapo wanaotumia taasisi za kisiasa na kidini kujaribu kuvuruga amani ya nchi. Hawa hatutawapa fursa hata kidogo kwa sababu amani ya nchi ikivurugika hakuna hata mmoja atakayebaki salama; sote tutaangamia,”alisema Rais Magufuli 

Aliwakumbusha wakazi wa Sengerema jinsi walivyowapokea wakimbizi kutoka nchi jirani ya Rwanda miaka ya tisini wakati taifa hilo lilipoingia kwenye mauaji ya kimbari yaliyoishia kwa watu zaidi ya milioni moja kupoteza maisha.

 “Tunayo mifano hai ya mataifa yaliyochezea amani na kusambaratika. Rwanda ilipitia njia hiyo kabla ya kusimama upya.Zipo Libya na Somalia ambazo hadi sasa zimegawanyika vipande vipande,” alisema Rais Magufuli. 

Aliwataka Watanzania kulinda kwa udi na uvumba amani na utulivu ulioasisiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na viongozi wengine, kwa kuwapiga vita wanaovuruga amani hata kama ni ndugu, jamaa, marafiki, wanachama au waumini wenzao. 

Rais anaendelea kutoa onyo hilo wakati Chadema ikiendelea kusisitiza maazimio ya Kamati Kuu ya chama hicho ya kuitisha mikutano ya hadhara nchi nzima kuanzia Septemba Mosi, ikiwa ni sehemu ya kampeni itakayoendeshwa na Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania (Ukuta), ambayo tayari baadhi ya wakuu wa mikoa wamepiga marufuku.

Chadema inadai kuwa uamuzi wa Rais kupiga marufuku mikutano ya kisiasa na kudhibiti wanasiasa kuhudhuria mikutano hiyo nje ya maeneo yao, ni kukiuka Katiba, Sheria ya Vyama vya Siasa, Kanuni za Maadili za Vyama vya Siasa na haki za binadamu.

Kuhusu vita dhidi ya ufisadi, Rais pia aliahidi kuongeza kasi kupitia mtindo wake wa kutumbua majipu, huku akilishukuru Bunge kwa kupitisha sheria itakayosaidia vita hivyo pamoja na kupitisha bajeti ya Sh2 bilioni ya kuanzisha Mahakama Maalumu ya Rushwa. 

Akizungumzia suala la chakula nchini, Rais John Magufuli amewaagiza wakuu wa mikoa na wilaya kuhakikisha maeneo yao yanazalisha chakula cha kutosha, akionya kuwa Serikali haitatoa chakula cha msaada kwa watakaokumbwa na njaa kutokana na uzembe na uvivu. 

Rais alisema kazi ya kulisha familia ni jukumu la wakuu wa familia na kuongeza kuwa kila familia ina wajibu kulima na kuhifadhi chakula cha kutosha mahitaji ya kipindi chote cha mwaka. 

“Kazi ya Serikali ni kutoa huduma kama barabara, dawa na mahitaji mengine ya kijamii, lakini si msaada wa chakula kwa watu wavivu,”alisema Rais Magufuli. 

Kuhusu usafiri wa Reli ya Kati, Rais alisema tayari Serikali imetengeneza zaidi ya Sh1 trilioni kwa ajili ya mradi wa kubadili reli hiyo kuwa katika viwango vya kimataifa. 

Alisema serikali pia inakusudia kununua meli mpya ya abiria itakayokuwa ikifanya safari Ziwa Victoria yenye uwezo wa kubeba abiria 1,000 na tani 800 ya mizigo. 

Pia alisema Serikali imeweka mikakati ya kukabiliana na uvuvi haramu kwenye Ziwa Victoria, ambalo lilikuwa likitoa fursa za ajira kwa watu zaidi ya milioni 6 katika nyanja mbalimbali, fursa ambazo alisema zimepungua maradufu kutokana vitendo vya uvuvi haramu. 

Rais Magufuli, ambaye atatumia ziara yake kukagua miradi ya maendeleo ikiwamo ujenzi wa daraja la juu la waenda kwa miguu eneo la Furahisha pamoja na upanuzi wa barabara ya Ghana-Pasiansi kutoka njia mbili za sasa hadi nne, leo anatahutubia mkutano wa hadhara kwenye viwanja vya Furahisha, Kirumba jijini Mwanza.


EmoticonEmoticon