Thursday, 11 August 2016

Aliyekuwa Akiibia Serikali Milioni 7 Kwa Dakika Akwama Kupata Dhamana

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imetupilia mbali maombi ya kufutwa kwa shitaka la utakatishaji fedha katika katika kesi ya kuisababishia serikali hasara ya Sh bilioni 14 inayomkabili, mfanyabiashara Mohammed Yusufali ‘Choma’ na mwenzake.
 
Hakimu Mkazi Mkuu Wilbard Mashauri alitoa uamuzi huo jana baada ya kupitia hoja zilizowasilishwa na pande zote mbili katika kesi hiyo.

 Kutokana na uamuzi huo, washitakiwa wataendelea kusota rumande hadi kesi itakapokwisha kwa kuwa kisheria mashitaka ya utakatishaji wa fedha hayana dhamana.
 
Katika kesi hiyo Choma aliyewahi kutajwa kujipatia Sh milioni saba kwa dakika moja kwa njia ya udanganyifu katika mapato ya serikali, pamoja na mfanyabiashara Samuel Lema, wanakabiliwa na mashitaka 222 ya kula njama, kutakatisha fedha, na kuisababishia serikali hasara hiyo kwa kukwepa kulipa kodi.
 
Akitoa uamuzi huo, Hakimu Mashauri alisema Mahakama imetupilia mbali maombi hayo yaliyowasilishwa na upande wa utetezi kwa kuwa haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo.
 
Alisema mahakama inakubali kuwa hati ya mashitaka inayowahusu washitakiwa hao haina makosa, hivyo Mahakama haiwezi kubadili hati hiyo kwa kuwa haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.
 
Aidha aliongeza kuwa, kama upande wa utetezi ungekuwa na nia ya kutaka kufutwa kwa shitaka hilo ungewasilisha maombi hayo tangu awali. Hakimu Mashauri aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 18, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.
 
Katika hoja za ombi hilo, Wakili wa utetezi Alex Mgongolwa aliomba shitaka hilo kufutwa kwa kuwa lina mapungufu kisheria na kuongeza kuwa si kila kosa la wizi na kughushi ni utakatishaji fedha, bali makosa yanayofuata baada ya vitendo hivyo yaani kuficha chanzo au asili ya upatikanaji wa fedha hizo ndiyo kosa la utakatishaji.
 
Alidai maelezo ya kwenye shitaka la 221 hayajengi kosa la utakatishaji fedha hivyo aliiomba mahakama ifute shitaka hilo ili waendelee na mashitaka mengine.
 
Upande wa Jamhuri uliiomba mahakama itupilie mbali ombi hilo kwa kuwa halina msingi kisheria na shitaka hilo lina maelezo ya kutosha kujenga kosa la utakatishaji wa fedha.
Read More

Hatimaye Dk Mwaka ajisalimisha Polisi


Siku chache baada ya Polisi wa Dar es Salaam kutangaza kumsaka mmiliki wa iliyokuwa kliniki ya tiba asilia ya Foreplan, Juma Mwaka ‘Dk Mwaka’ kwa agizo la Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Hamis Kigwangallah, tabibu huyo ameamua kujisalimisha polisi.

Dk Kiwangallah alitoa agizo hilo siku sita zilizopita baada ya kutembelea kliniki hiyo kwa mara ya pili. Dk Mwaka alijisalimisha jana saa nne asubuhi katika Kituo cha Kikuu cha Polisi, jijini Dar es Salaam na kuhojiwa kwa saa kadhaa kabla ya kuachiwa kwa dhamana. 

Msako wa Dk Mwaka unachagizwa na madai ya ukiukwaji wa agizo la Serikali la kuendelea na utoaji wa tiba licha ya kufungiwa. 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, Salum Hamdani alisema jana kuwa baada ya kujisalimisha muda huo, alihojiwa na kuachiwa kwa dhamana lakini akatakiwa kuripoti leo kwa mahojiano zaidi. 

“Kuhusu kupelekwa mahakamani, ni mpaka jeshi la Polisi litakapomaliza kukusanya ushahidi na kumkabidhi DPP ambaye atautumia kufungua kesi,” alisema.

Read More

CCM, AG na IGP 'Wagoma' Kushiriki Kikao cha Kujadili UKUTA Wa Chadema Kilichoitishwa na Tume ya Haki na Utawala Bora


MKUU wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali (IGP), Ernest Mangu, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju, hawakutokea kwenye mkutano ulioandaliwa na Tume ya Haki na Utawala Bora jijini Dar es Salaam jana.

Mkutano uliokuwa na lengo la kumaliza mvutano ulioibuka kati ya vyombo vya dola na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Mvutano huo unatokana na amri ya Rais John Magufuli, ya kupiga marufuku kufanyika kwa maandamano na mikutano ya vyama vya siasa hadi mwaka 2020.

Rais Magufuli, hata hivyo, ameruhusu viongozi waliochaguliwa kama madiwani na wabunge kufanya mikutano kwenye maeneo waliyopigiwa kura.

Kupinga amri hiyo, Chadema kimeamua kuitisha maandamano na mikutano ya wanachama na wafuasi wao nchi nzima yatakayofanyika, Septemba mosi, mwaka huu katika operesheni waliyoipa jina la `Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania’ (Ukuta).

Baada ya kuibuka kwa mvutano huo, uliosababisha Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu kukamatwa na Jeshi la Polisi na kufunguliwa mashtaka ya uchochezi, tume hiyo iliwaita IGP Mangu, Kinana, Masaju, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, Katibu Mkuu wa Chadema, Vincent Mashinji na Mkurugenzi wa Taasisi ya Demokrasia (TCD), Daniel Loya.

Hata hivyo, IGP Mangu, Kinana na Masaju hawakuhudhuria mkutano huo kutokana na kile kilichoelezwa kuwa walitoa udhuru.

Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Bahame Nyanduga, alisema jijini jana kuwa wametoa mapendekezo matatu ambayo yanapaswa kufuatwa na pande zote zinazovutana.

Alisema mapendekezo yao yamelenga kutoa nafasi kwa mahakama kuamua kesi zilizofunguliwa.

Nyanduga aliyataja mapendekezo hayo kuwa ni Jeshi la Polisi na Chadema kusitisha matumizi ya lugha au maneno yenye viashiria vya uvunjifu wa amani, haki za binadamu na utawala bora kwa kuwa lugha hizo hazikidhi matakwa ya sheria.

Alisema wamependekeza Jeshi la Polisi linapaswa kutokutumia maneno "tutawashughulikia wote watakaokaidi amri" kwa kuwa tume inaamini kuwa matumizi ya maneno hayo yanaweza kusababisha matumizi mabaya ya mamlaka ya jeshi hilo.

“Ni katika mazingira haya, tume imepata wasiwasi kuwa endapo matamko haya yataachiwa yaendelee, yana viashiria vya machafuko na uvunjifu mkubwa wa haki za binadamu unaoweza kutokea,” alisema Nyanduga.

Alisema pendekezo lingine ni Chadema kurekebisha msamiati wa mikutano wanayopanga na kuondoa neno udikteta katika mikakati yao ya kisiasa.

Akifafanua kuhusu pendekezo hilo, Nyanduga alisema Tanzania ni nchi yenye taasisi za kidemokrasia na inaheshimu utawala wa sheria na ndiyo sababu Chadema wamekwenda mahakamani.

Alisema Chadema na Jeshi la Polisi wanapaswa kuheshimu mahakama na kuacha kutoa matamko ambayo yanaendelea kuongeza joto kuhusu uwapo au kutokuwapo maandamano na mikutano ya Septemba Mosi, mwaka huu.

Nyanduga alisema pendekezo la tatu ni Chadema kusitisha maandamano yake ili kutoa nafasi kwa mahakama kufanya kazi yake kwa umakini bila shinikizo la muda kuanzia sasa hadi Septemba Mosi.

Alisema kutozingatiwa kwa mapendekezo hayo kutasababisha kutokea kwa uvunjifu wa haki za binadamu na jambo hilo likitokea, wahusika wote watawajibishwa.

Alisema tume ina mamlaka ya kujadili hoja hizo mbili kwa kuzingatia mamlaka iliyonayo chini ya Ibara 130 (1) (g) na (h) ya Katiba ya nchi, kuhusu kutoa ushauri na kutafuta maelewano kati ya viongozi wa serikali na Jeshi la Polisi kwa upande mmoja na uongozi wa Chadema.

Nyanduga aliongeza kuwa mkutano wa jana ulikuwa na lengo la kuzungumzia tamko la Jeshi la Polisi la kuzuia mikutano na maandamano ya vyama vya siasa isiyo ya kiutendaji na tamko la Chadema kuhusu Ukuta.

“Ofisi ya AG, IGP na CCM tuliwaalika, lakini walitujibu kuwa hawataweza kuhudhuria kwa kuwa wana udhuru, hivyo tulikutana na Chadema, Ofisi ya Msajili na TCD (Kituo cha Demokrasia Tanzania), na kukubaliana kutafanyika kikao kuhusu umuhimu wa kudumisha amani nchini,” alisema Nyanduga.

Julai 27, mwaka huu, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alitangaza kuzinduliwa kwa Operesheni Ukuta kwa lengo la chama hicho kufanya mikutano nchi nzima ifikapo Septemba Mosi mwaka huu, baada ya amri ya Rais Magufuli na Jeshi la Polisi kuzuia kufanyika kwa mikutano ya kisiasa na maandamano nchini.

Mashinji Afunguka
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Mashinji, alipotafutwa ili kueleza juu ya mapendekezo ya tume, alisema anashangaa kuambiwa kwamba kuna masuala yaliyojadiliwa kwa kuwa kikao hakikufanyika jana.

“Mbona hicho kikao hakijafanyika? "alihoji. "Kulikuwa na mvutano kwamba kifanyike ama kisifanyike kwa sababu akidi haikutimia, nashangaa kusikia kuna maazimio yamepitishwa.

“Hiyo inaonyesha kabisa ni njama za hao watu ili ionekane kuna kikao kilifanyika, kikao kisingeweza kufanyika kwa sababu hawakuwapo Kinana, IGP, wala AG,” alisema Dk. Mashinji.

Alisema anachojua yeye ni kwamba, wao wanaendelea kama kawaida na maandalizi yao ya mikutano ya hadhara na maandamano nchi nzima hiyo Septemba 1, mwaka huu.
Read More

Kauli ya serikali kuhusu kuhamishwa kwa stendi ya mabasi Ubungo Jijini Dar es Salaam

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amewapiga marufuku mawakala wanaotoza faini za kuegesha magari vibaya katika Kituo Kikuu cha Mabasi yaendayo Mikoani cha Ubungo hadi hapo yatakapotengenezwa maeneo rasmi kwa ajili ya maegesho ya magari.

Makonda alitoa kauli hiyo jana wakati alipofanya ziara kujionea hali halisi ya kituo hicho.

Alisema haiwezekani mawakala wakaendelea kutoza faini za maegesho ambayo si sahihi wakati katika eneo hilo hakuna maeneo maalumu kwa ajili ya maegesho ya magari.

“Nataka maeneo rasmi yakishatengwa ndipo muanze kutoza faini, mmekuwa mkiwasumbua wananchi hawajui wapi ni sehemu ya maegesho na wapi si sehemu ya maegesho wekeni alama ndipo muanze kuwatoza,” alisema Makonda.

Licha ya kutoa kauli hiyo, Makonda pia alimtaka Mkurugenzi wa Jiji kabla ya kumalizika wiki hii kuhakikisha kituo hicho kinawekwa taa ili kuondoa usumbufu wanaokutana nao abiria na wananchi hasa wakati za usiku.

"Lakini kabla ya wiki hii haijaisha nataka kuona taa zote za ubungo zinawaka, sitaki kuviona vifusi katika eneo hili la stendi na baada ya siku 20 nitarejea kujionea utekelezaji wake kama umekamilika"  Alisema Makonda

Katika hatua nyingine, Makonda alisema kuwa serikali ipo katika mpango mwisho wa kuihamishia stendi hiyo kutoka ubungo kwenda Mbezi mwisho.

"Shahuku yangu ni kuwa na stendi tofauti na tuliyonayo, nataka Dar es salaam iwe na stendi ya kimataifa na tayari tunalo eneo kule mbezi ambapo halmashauri ya jiji tayari ipo kwenye mchakato wa kukamilisha ujenzi huo.

"Nataka kuihamisha hii stendi ya ubungo ili tuepukane na kero ya kukutana na mabasi ya mwendo kasi kwakuwa nayo ni moja ya changamoto, duniani kote maroli  yakiingia katikati ya mji hutumika kubeba mikate ajabu Dar es salaam maroli yanabeba ngano na makontena"
Read More

Kitwanga Akutana Uso Kwa Uso na Rais Magufuli

Rais John Magufuli jana alikutana ana kwa ana na rafiki yake, Charles Kitwanga ikiwa ni siku 80 baada ya kumvua cheo cha Waziri wa Mambo ya Ndani kwa kosa la kuingia bungeni kujibu maswali akiwa amelewa. 

Wawili hao walikutana kwenye Jimbo la Misungwi ambako Rais alisimama akitokea Wilaya ya Sengerema ambako alihutubia wananchi. 

Rais alitengua uteuzi wa Kitwanga Mei 20, wakati sakata la utekelezwaji mbovu wa mkataba wa Sh37 bilioni baina ya Jeshi la Polisi na kampuni ya Lugumi Enterprises likivuma kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano. 

Lakini jana, hali ilionekana ya kikazi zaidi wakati Rais alipofika kwenye jimbo hilo. Kitwanga, ambaye ni mbunge wa Misungwi mkoani Mwanza, alitumia nafasi hiyo kukutana na Rais kwa mara ya kwanza hadharani, kuwasilisha kero za wananchi wake, hasa ya maji. 

Katika tukio hilo lililovutia hisia za waliokuwepo, Rais aliuthibitishia umma kuwa yeye na Kitwanga ni marafiki wa muda mrefu, alipokuwa akijibu ombi la mbunge huyo la kutaka Serikali itatue kero ya maji eneo la Usagara na Misungwi. 

“Kitwanga ni rafiki yangu. Tayari Serikali imepanga kutumia zaidi ya Sh8 bilioni kutekeleza mradi mkubwa wa maji maeneo ya jimbo la Misungwi, ikiwemo Usagara,” alisema Rais Magufuli akiwa amesimama kwenye gari lililofunuliwa upande wa juu. 

Katika sakata la Lugumi, wabunge walitaka suala lijadiliwe baada ya taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kubaini kuwa kampuni hiyo ilishindwa kufunga mashine za kielektroniki za kuchukulia alama vidole kwa mujibu wa mkataba. 

Mkataba huo ulisainiwa mwaka 2011 lakini hadi CAG alipokuwa akifanya ukaguzi mwaka jana, ni vituo 14 tu kati ya 118 vilivyokuwa vimefungwa mashine hizo, huku Lugumi Enterprises ikiwa imelipwa Sh36 bilioni ambazo ni zaidi ya asilimia 90 ya fedha za mkataba huo. 

Kitwanga alihusishwa na sakata hilo kutokana na dhamana yake na pia kuwa na hisa kwenye kampuni ya Infosys, ambayo ni wakala wa kampuni ya Dell inayozalisha kompyuta, kuhusishwa kutoa vifaa hivyo. 

Hata hivyo, Juni 22, Kitwanga aliwaambia waandishi wa habari nyumbani kwake kuwa Infosys haina uhusiano wowote wa kibiashara na Lugumi.

Jitihada za wabunge, hasa wa upinzani kutaka kuzungumzia suala hilo zilikwama kwa maelezo ya kutaka kusubiri ripoti ya kamati ndogo iliyoundwa kuchunguza suala hilo. 

Ripoti hiyo iliwasilishwa mwishoni mwa vikao vya Bunge la Bajeti na haikujadiliwa baada ya Naibu Spika, Dk Tulia Ackson kusoma maagizo ya Bunge kwa pande zinazohusika kwenye mkataba. 

Kabla ya suala hilo kuzuiwa kujadiliwa, wabunge walikuwa wakidai kuwa Rais na Kitwanga ni marafiki wa karibu na baadaye mitandao ya kijamii ikasambaza mkanda unaoonyesha jinsi walivyokuwa wakijadili suala la Magufuli kuchukua fomu ya kugombea urais. 

Kwenye kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, Magufuli alimnadi Kitwanga kwa kueleza kuwa anamfahamu kwa kuwa walisoma wote na ni rafiki yake. 

Kabla ya kwenda Sengerema kwa kivuko jana, Rais alihutubia wilayani Sengerema ambako aliendelea na onyo lake dhidi ya watu anaosema wanataka kuvuruga amani.

Akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Mnadani mjini Sengerema, Rais Magufuli aliwataka wenye lengo la kuvuruga amani kumsubiri amalize kipindi chake cha uongozi kwa sababu hatawapa fursa hiyo. 

“Wapo wanaotumia taasisi za kisiasa na kidini kujaribu kuvuruga amani ya nchi. Hawa hatutawapa fursa hata kidogo kwa sababu amani ya nchi ikivurugika hakuna hata mmoja atakayebaki salama; sote tutaangamia,”alisema Rais Magufuli 

Aliwakumbusha wakazi wa Sengerema jinsi walivyowapokea wakimbizi kutoka nchi jirani ya Rwanda miaka ya tisini wakati taifa hilo lilipoingia kwenye mauaji ya kimbari yaliyoishia kwa watu zaidi ya milioni moja kupoteza maisha.

 “Tunayo mifano hai ya mataifa yaliyochezea amani na kusambaratika. Rwanda ilipitia njia hiyo kabla ya kusimama upya.Zipo Libya na Somalia ambazo hadi sasa zimegawanyika vipande vipande,” alisema Rais Magufuli. 

Aliwataka Watanzania kulinda kwa udi na uvumba amani na utulivu ulioasisiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na viongozi wengine, kwa kuwapiga vita wanaovuruga amani hata kama ni ndugu, jamaa, marafiki, wanachama au waumini wenzao. 

Rais anaendelea kutoa onyo hilo wakati Chadema ikiendelea kusisitiza maazimio ya Kamati Kuu ya chama hicho ya kuitisha mikutano ya hadhara nchi nzima kuanzia Septemba Mosi, ikiwa ni sehemu ya kampeni itakayoendeshwa na Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania (Ukuta), ambayo tayari baadhi ya wakuu wa mikoa wamepiga marufuku.

Chadema inadai kuwa uamuzi wa Rais kupiga marufuku mikutano ya kisiasa na kudhibiti wanasiasa kuhudhuria mikutano hiyo nje ya maeneo yao, ni kukiuka Katiba, Sheria ya Vyama vya Siasa, Kanuni za Maadili za Vyama vya Siasa na haki za binadamu.

Kuhusu vita dhidi ya ufisadi, Rais pia aliahidi kuongeza kasi kupitia mtindo wake wa kutumbua majipu, huku akilishukuru Bunge kwa kupitisha sheria itakayosaidia vita hivyo pamoja na kupitisha bajeti ya Sh2 bilioni ya kuanzisha Mahakama Maalumu ya Rushwa. 

Akizungumzia suala la chakula nchini, Rais John Magufuli amewaagiza wakuu wa mikoa na wilaya kuhakikisha maeneo yao yanazalisha chakula cha kutosha, akionya kuwa Serikali haitatoa chakula cha msaada kwa watakaokumbwa na njaa kutokana na uzembe na uvivu. 

Rais alisema kazi ya kulisha familia ni jukumu la wakuu wa familia na kuongeza kuwa kila familia ina wajibu kulima na kuhifadhi chakula cha kutosha mahitaji ya kipindi chote cha mwaka. 

“Kazi ya Serikali ni kutoa huduma kama barabara, dawa na mahitaji mengine ya kijamii, lakini si msaada wa chakula kwa watu wavivu,”alisema Rais Magufuli. 

Kuhusu usafiri wa Reli ya Kati, Rais alisema tayari Serikali imetengeneza zaidi ya Sh1 trilioni kwa ajili ya mradi wa kubadili reli hiyo kuwa katika viwango vya kimataifa. 

Alisema serikali pia inakusudia kununua meli mpya ya abiria itakayokuwa ikifanya safari Ziwa Victoria yenye uwezo wa kubeba abiria 1,000 na tani 800 ya mizigo. 

Pia alisema Serikali imeweka mikakati ya kukabiliana na uvuvi haramu kwenye Ziwa Victoria, ambalo lilikuwa likitoa fursa za ajira kwa watu zaidi ya milioni 6 katika nyanja mbalimbali, fursa ambazo alisema zimepungua maradufu kutokana vitendo vya uvuvi haramu. 

Rais Magufuli, ambaye atatumia ziara yake kukagua miradi ya maendeleo ikiwamo ujenzi wa daraja la juu la waenda kwa miguu eneo la Furahisha pamoja na upanuzi wa barabara ya Ghana-Pasiansi kutoka njia mbili za sasa hadi nne, leo anatahutubia mkutano wa hadhara kwenye viwanja vya Furahisha, Kirumba jijini Mwanza.

Read More

Mtuhumiwa Auawa Ndani ya Kituo cha Polisi


MKAZI wa Kwere wilayani Babati Mkoa wa Manyara, Mohamedy Pagweje (29), amepigwa na kufa na mtu anayedaiwa kuwa hana akili timamu aliyewekwa naye katika chumba cha mahabusu katika Kituo cha Polisi cha Mkoa wa Manyara, kilichopo wilayani Babati.

Hata hivyo, ndugu wa Pagweje ambaye ni fundi ujenzi wa eneo hilo, wamekataa kuuchukua mwili kwa maziko wakitaka kujua ukweli wa kifo chake baada ya kupigwa akiwa mahabusu katika Kituo cha Polisi cha Babati.

Mama mzazi wa kijana huyo Hadija Pagweje, akizungumza na waandishi wa habari jana nje ya ofisi ya Mkuu wa Wilaya hiyo, Raymond Mushi, alisema alimkabidhi mtoto wake kituoni hapo saa 8:00 mchana juzi akiwa salama.

Alisema alimfikisha mwanawe kituoni hapo baada ya kijana huyo kulewa pombe na kutishia kujiua kutokana na kutolipwa fedha za ujenzi kutoka kwa askari aliyemjengea nyumba. Askari huyo ametajwa kwa jina moja la Justine.

“Nilimwacha hapa kituoni mahali pa usalama na kuwaomba askari wa zamu wanisaidie maana kijana wangu amekunywa pombe nyingi, anatishia kujiua kwa madai kuwa amekosa haki yake. Nilifanya hivyo nikijua kituo cha polisi kina usalama ili angalau pombe ziishe, jioni nimchukue,” alisema.

Alipokwenda kupeleka chakula polisi walimtaka arudi tena saa 12:00 jioni, aliporudi kituoni hapo alishangaa kuona baadhi ya watu wakimshangaa na kumjulisha kuwa kijana wake amepigana na mahabusu mwenzie na kuwa amepelekwa Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Babati ya Mrara kwa matibabu.

Alisema alipokwenda katika hospitali hiyo alikutana na askari ambaye alimfahamisha kuwa mtoto wake alikuwa amefariki dunia. Baba wa marehemu Amiri Shabani alisema alipata taarifa ya kifo cha kijana wake saa 1:00 usiku juzi baada ya kuelezwa kuwa mtoto wake alikufa akiwa anadai Sh 200,000 kutoka kwa askari huyo.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Francis Massawe alikiri kutokea kwa tukio hilo, saa 8:00 mchana Agosti 8, mwaka huu ambapo alisema mama wa marehemu alimpeleka kituoni hapo kijana wake Pagweje, fundi ujenzi akidai kuwa alikuwa akimletea fujo na alifunguliwa mashtaka ya kutishia kuua.

Alipoingizwa mahabusu alipigana na mahabusu mwenzake Bura Malireh (19) mkulima na mkazi wa Gijedaboung Kata ya Mamire wilayani humo, ambaye ilidaiwa alikuwa mgonjwa wa akili.
Read More

Taarifa Toka IKULU Kuhusu Ziara ya Rais Magufuli Jijini Mwanza Iliyoanza Jana

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli  tarehe 10 Agosti, 2016 ameanza ziara ya siku mbili katika mikoa ya Geita na Mwanza baada ya kumaliza mapumziko mafupi nyumbani kwake Chato Mkoani Geita.

Jijini Mwanza Rais Magufuli alipokelewa na maelfu ya wananchi waliokuwa wakisimamisha msafara wake tangu alipoingia kupitia kivuko cha Busisi - Kigongo na baadaye kupita Usagara, Buhongwa, Mkolani, Nyegezi, Mkuyuni na Igogo ambako pamoja na kuwahakikishia kuwa Serikali yake imejipanga kukabiliana na kero mbalimbali za wananchi na kuwaletea maendeleo, amesitisha agizo la Jiji la Mwanza la kuwataka wafanyabiashara wadogo maarufu kwa jina la Machinga kutofanya biashara zao katikati ya Jiji ifikapo tarehe 20 Agosti, 2016.

Pamoja na kusitisha agizo hilo, Dkt. Magufuli amewaagiza viongozi wa Jiji la Mwanza na Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela kutafuta na kuandaa maeneo ambayo wafanyabiashara hao watayatumia kwa ajili ya kufanyia biashara zao.

"Na mtakapowatafutia maeneo ya biashara wapelekeni sehemu ambazo ni nzuri, msiwapeleke sehemu ambazo hazina biashara, hawa wamachinga wanaendesha maisha yao kwa kutumia biashara hizi"Amesema Rais Magufuli.

Aidha, Rais Magufuli amewahakikishia wananchi wa Mwanza kuwa Serikali imeanza kufanya usanifu na upembuzi yakinifu ikiwa ni maandalizi ya kuanza ujenzi wa daraja kubwa litakalounganisha eneo la Busisi Wilayani Sengerema na Kigongo Wilayani Misungwi ili kuondoa adha ya wananchi kuvuka eneo hilo kwa kutegemea vivuko, na pia itahakikisha inanunua meli moja katika ziwa viktoria kama ilivyoahidi.

Kabla ya kuingia Jijini Mwanza Rais Magufuli alihutubia mkutano wa hadhara katika Mji wa Sengerema na pia alizungumza na wananchi wa Sima Wilayani Sengerema na Kasamwa Wilayani Geita ambako aliwahakikishia kuwa Serikali yake itaongeza msukumo katika kutatua tatizo la uhaba wa maji katika maeneo hayo kwa kusambaza maji ya kutoka ziwa Viktoria huku akiwataka viongozi halmashauri husika kutumia rasilimali za halmashauri kutatua tatizo hilo la maji katika maeneo ambayo hayatapitiwa na mradi mkubwa wa maji ya kutoka ziwa Viktoria.

Katika hatua nyingine Mhe. Rais Magufuli amewaagiza viongozi wa Mikoa ya Mwanza na Geita kutafakari sababu zilizosababisha kufa kwa Chama Kikuu cha Ushirika cha NYANZA na viwanda vya kuchambua pamba (Ginneries) ili kupanga namna ya kuvifufua.

Rais Magufuli alitoa agizo hilo  alipokuwa akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Kasamwa kilichopo Wilayani Geita na ameahidi kuwa Serikali yake ipo tayari kuunga mkono juhudi za wakulima kwa kuanzisha viwanda vya kuongeza thamani ya mazao yao ikiwemo zao la pamba.

Rais Magufuli atakamilisha ziara yake ya siku mbili leo tarehe 11 Agosti, 2016 kwa kuweka jiwe la msingi katika Daraja la watembea kwa miguu na kuzungumza na wananchi wa Mwanza katika Uwanja wa Furahisha.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Mwanza

10 Agosti, 2016
Read More

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akabidhiwa mpango wa kuhamia Dodoma

MKOA wa Dodoma wakishirikiana na Mamlaka ya Ustawishaji wa Makao Makuu (CDA) wametekeleza agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa la kuandaa na kuwasilisha mapendekezo ya awali ya namna serikali itakavyohamia Dodoma.

Aidha, imeelezwa kuwa kuanzia sasa Waziri Mkuu ataweka hadharani maelekezo ya wizara na watumishi kuhamia Dodoma.

Hayo yamebainishwa katika mahojiano yaliyofanyika jana  na Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma, Rehema Madenge.

Mwishoni mwa mwezi uliopita, Waziri Mkuu wakati akizungumza na viongozi wa serikali, taasisi, watendaji na wananchi wa Mkoa wa Dodoma alielezea azma ya serikali kuhamia Dodoma na kutoa siku 14 kwa Mkoa na CDA, kuwasilisha mapendekezo ya awali kwa namna serikali itakavyohamia Dodoma.

Akitoa siku hizo kwa Serikali ya Mkoa wa Dodoma kukaa na taasisi zake, hususani CDA kuandaa na kutoa mpango kazi wake, Majaliwa alisema, “Ndani ya siku 14 nipate proposal (mapendekezo) ya kwanza namna mtakavyotekeleza, naagiza kiundwe kikosi kazi chini yenu kitakachowajumuisha makundi yote. Baada ya siku 14 nipate mpango wenu.”

Madenge alisema kwamba Mkuu wa Mkoa huo, Jordan Rugimbana yuko Dar es Salaam alitarajiwa kuwasilisha mpango kazi huo kwa Waziri Mkuu na kwamba muda wowote Waziri Mkuu atatangaza utaratibu wa kuhamia Dodoma.

“Tumeandaa mpango kazi kulingana na maelekezo ya waziri mkuu na mkuu wa mkoa amekwenda kukabidhi mpango huo,” alisema Katibu Tawala Dodoma.

Akizungumzia taarifa za baadhi ya wizara kuanza kuhamia huko, Katibu tawala huyo alisema kwamba kama mkoa hawana taarifa za wizara na watumishi kuanza kuhamia Dodoma.

“Tunasubiri maelekezo ya waziri mkuu, baada ya mpango kazi kukamilika utawekwa hadharani mambo yote ya serikali kuhamia Dodoma,” alisema Madenge. 

Akifafanua zaidi, alisema anachojua yeye mpango unakabidhiwa Ofisi ya Waziri Mkuu na na wizara zitajipanga kwa mujibu wa maelekezo ya Waziri Mkuu Majaliwa.

Mkoa wa Dodoma umekuwa katika hekaheka za kutekeleza maagizo ya serikali ya kuhamia Dodoma, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba huduma muhimu kama upatikanaji wa viwanja zinakwenda kwa taratibu zinazotakiwa.

Ili kuondoa mhemko na udalali wa viwanja unaoweza kupandisha bei na pia kuzuia vurugu, mkuu wa mkoa amepiga marufuku uuzaji wa viwanja ndani ya mji wa Dodoma. Sababu kubwa ya kupiga marufuku kunatokana na kundi la madalali kutoka mikoa mbalimbali kuvamia mji.

Kupokewa kwa mpango kazi huo ni moja ya hatua za kukamilisha uhamiaji wa serikali Dodoma, ambapo hatua nyingine ni kwa serikali kuwasilisha bungeni muswada wa kuitambua Dodoma kama makao makuu ya nchi ili uthibitishwe kisheria.

Muswada huo utawasilishwa katika Bunge linaloanza Septemba 6, mwaka huu.

Waziri Mkuu Majaliwa alisema muswada huo wa sheria ya serikali kuhamia Dodoma, utapelekwa bungeni ili azma ya Rais John Magufuli na serikali yake uwe na nguvu kisheria, baada ya Rais Magufuli kutangaza hivi karibuni kuwa ndani ya miaka minne na ushee iliyobaki ya kumaliza muhula wake wa kwanza wa urais, Serikali ya Awamu ya Tano itakuwa imehamia katika mji wa Dodoma, ambao mwaka 1973 ulitangazwa kuwa Makao Makuu ya Tanzania.
Read More

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Alhamisi ya Agosti 11


Read More

Rais Magufuli Aanza Ziara Yake Mkoani Mwanza.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongella mara baada ya kuwasili katika Wilaya ya Sengerema Mkoani Mwanza.

  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akihutubia mamia ya wakazi wa Sengerema mkoani Mwanza mara baada ya kuwasili akitokea Chato mkoani Geita.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwapungia wanakwaya wa UWT Kisima cha maji Chumvi mara baada ya kuhutubia wakazi wa Sengerema mkoani Mwanza.
  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na Mwalimu Mstaafu wa Shule ya Sekondari Sengerema Wilson Fumbuka Mbanga ambaye walifundisha naye shule hiyo tokea mwaka 1982-1985 mara baada ya kumaliza mkutano wa hadhara Sengerema Mkoani Mwanza.


 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiaagana na wakazi wa Sengerema mkoani Mwanza mara baada ya kumaliza kuwahutubia.
  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akihutubia wakazi wa Busisi wakati akielekea Mwanza.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa ndani ya kivuko cha MV. Misungwi wakati akielekea mkoani Mwanza. 
PICHA NA IKULU.
Read More

Wednesday, 10 August 2016

Habari Zilizopo Katika Magazeti Ya Leo Jumatano ya Agosti 10

Read More